All news

Community Outreach

Mahojiano Maalum Radio Joy FM Kigoma — Kutambulisha Malka Foundation Helper

18 June 2026 · Kigoma Region, Tanzania

Timu ya Malka Foundation Helper Mkoa wa Kigoma ilipata fursa ya kutembelea studio za Radio Joy FM Kigoma pamoja na mmoja wa wanufaika wa Kikundi cha Mabinti Wajasiriamali wa Simbo kwa ajili ya mahojiano maalum.

Katika mahojiano hayo, tulipata nafasi ya kuitambulisha Malka Foundation Helper kwa jamii, kuelezea shughuli mbalimbali tunazotekeleza Mkoa wa Kigoma, pamoja na mafanikio yanayopatikana kupitia programu zetu za kuwawezesha wanawake, vijana na watoto.

Mahojiano hayo yalienda sambamba na kampeni ya uhamasishaji yenye kaulimbiu ya: “Introducing Malka Foundation Helper to the communities and awareness campaign of Empowering Communities Through Skills, Education and Opportunities.” Kupitia ujumbe huo, tuliwahamasisha wasikilizaji kutambua umuhimu wa ujuzi wa vitendo, elimu jumuishi na fursa za kiuchumi katika kujenga jamii imara na zinazojitegemea.

Aidha, tulipata fursa ya kutangaza na kuonesha baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na mabinti wa Kikundi cha Wajasiriamali cha Simbo baada ya kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji. Bidhaa hizo ni pamoja na sabuni za maji na bidhaa nyingine za usafi zinazowawezesha mabinti hao kuongeza kipato na kujitegemea kiuchumi.

Kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za mabinti hao, timu ya Malka Foundation Helper ilikabidhi zawadi ya bidhaa hizo kwa uongozi wa Radio Joy FM. Hatua hiyo ilizaa matokeo chanya ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Radio Joy FM alitoa oda maalum ya kununua chupa 12 za sabuni za maji za lita 3, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za mabinti hao na kuwapa moyo wa kuendelea kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko.

Ziara na mahojiano haya yameendelea kufungua mlango wa ushirikiano kati ya jamii, vyombo vya habari na vikundi vya wanufaika wetu, huku yakiongeza mwonekano wa kazi ya Malka Foundation Helper katika kuleta mabadiliko chanya kupitia ujuzi, elimu na fursa.

Support agent