Day of the African Child
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika — Shule ya Sekondari UAMUZI
4 June 2026 · Dar es Salaam, Tanzania
Tarehe 04 Juni 2026, Malka Foundation Helper ilifanikiwa kuendesha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika jijini Dar es Salaam, katika Shule ya Sekondari UAMUZI.
Shughuli ilianza kwa utambulisho wa Malka Foundation Helper na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi yetu. Utambulisho huo uliongozwa na mkurugenzi wetu Bi. Tabu Ally Kilonge, ambaye alieleza dhamira na malengo ya taasisi katika kuwawezesha watoto, vijana na jamii kwa ujumla.
Mada kuu ya maadhimisho ilijikita katika kaulimbiu ya mwaka huu 2026 inayosema: "Mtoto ni malezi na msingi wa familia bora kwa taifa imara." Kupitia mada hii, wanafunzi walipata elimu kuhusu umuhimu wa malezi bora, wajibu wa wazazi na walezi, changamoto zinazowakabili watoto katika jamii pamoja na namna ya kujenga mazingira salama na rafiki kwa maendeleo yao.
Katika kuonesha kuwa kushiriki ni kujali, Malka Foundation Helper pia ilishiriki chakula na wanafunzi. Kipengele hiki cha pamoja kilileta furaha kubwa na kukumbusha kuwa malezi bora hayaonekani kwa maneno tu, bali pia kwa matendo ya upendo, ukarimu na kujali ustawi wa mtoto.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuongezeka kwa uelewa wa wanafunzi kuhusu malezi bora, haki za mtoto na wajibu wao katika kujenga mustakabali bora. Wanafunzi walionesha furaha na shauku kubwa ya kuendelea kushiriki katika programu za elimu na maendeleo zinazoendeshwa na Malka Foundation Helper.
Kwa ujumla, shughuli imefanyikiwa kwa mafanikio makubwa na tumekubaliana kuendelea kushirikiana na wanafunzi kupitia Gender Club na programu nyingine za kuwawezesha watoto na vijana.
Pia tulibaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi, ikiwemo ukali wa kupita kiasi kutoka kwa baadhi ya wazazi na walezi. Kwa upande wa shule, tuliona mahitaji ya vifaa vya michezo, upanuzi wa maktaba pamoja na ongezeko la rafu za kuhifadhia vitabu na vifaa vya kujifunzia.

