Day of the African Child
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika — Simbo 2026
12 June 2026 · Simbo, Kigoma, Tanzania
Tarehe 12 Juni 2026, Malka Foundation Helper Mkoa wa Kigoma — kwa ushirikiano na Serikali ya Kata ya Simbo na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma — ilifanikiwa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika katika Kijiji cha Simbo. Maadhimisho hayo yalihusisha watoto, vijana na wanajamii mbalimbali katika siku ya furaha, elimu na malezi.
Kama sehemu ya wadau wakuu wa maadhimisho hayo, Malka Foundation Helper iliratibu na kuendesha michezo mbalimbali kwa watoto iliyolenga kujenga ushiriki, furaha na kuimarisha mahusiano miongoni mwa watoto. Watoto walionesha vipaji mbalimbali kupitia michezo, nyimbo na burudani zilizopamba maadhimisho hayo.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Malka Foundation Helper, Bi. Tabu Ally, alipata nafasi ya kuwasilisha taarifa ya shughuli zinazotekelezwa na taasisi katika Kata ya Simbo, pamoja na kueleza miradi ya maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa katika kipindi kijacho. Nakala ya taarifa hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya taarifa na ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Ujumbe mkuu wa maadhimisho uliendelea kuonesha kuwa mtoto ndiye msingi wa familia bora na taifa imara. Watoto walishiriki kwa furaha kupitia maandamano mafupi ya uhamasishaji, mabango ya mikono, nyimbo na shughuli za pamoja zilizosisitiza haki za mtoto na wajibu wa jamii katika kumlinda na kumlea.
Picha na ushiriki mkubwa wa washiriki vinaonesha moyo wa pamoja wa kuendelea kushirikiana katika programu za maendeleo ya watoto na vijana katika eneo la Simbo na Kigoma kwa ujumla.

